Umekuwa Imanueli, ni Mungu pamoja nami
Daima wewe mkweli, uongo katu husemi
Na katika zote hali, kunibariki hukomi
Mungu ninapokuwaza, ninakutabasamia
Wewe ni muaminifu, kwa kila unachosema
Meniondolea hofu, na ukanitenda mema
Sijapata hitilafu, kwangu Umekuwa mwema
Mungu ninapokuwaza, ninakutabasamia
Mwanao ninakupenda, nami nitakuishia
Kote nitakapoenda, sifa nitakupatia
Mimi kamwe sitapenda, utukufu kuchukua
Mungu ninapokuwaza, ninakutabasamia
Maneno hayatatosha, wewe kukuandikia
Machozi hayataisha, kwa vile mefurahia
Ewe Mungu menikosha, mimi ninakuinua
Mungu ninapokuwaza, ninakutabasamia
kutoka kwa bintio :Mchele wa chenga